Italia kwamkubali Romelu Lukaku, atupia mbili wakati Inter ikitoa sare ya 2 – 2 na Borrusia Monchengladbach

Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Chelsea na Everton na sasa Inter Milan Romelu Lukaku anaonekana kuendelea kuiva na kuwa hatari zaidi karibu na lango la mpinzani baada ya jana kukiokoa kikosi cha timu yake kutopoteza mechi dhidi ya Borrusia Monchengladbach kwa goli lake la dakika za lala salama hatua ya makundi ya Uefa.

Katika dakika ya 90 ya mchezo, Lukaku alitupia bao lililoipa timu yake alama moja likiwa ni bao lake la pili katika mchezo huo baada ya kuitanguliza Inter kwa goli la mapema kipindi cha pili kabla ya mambo kuwageukia, bao hilo lilikuwa la nane kwenye mechi 8 ambazo amecheza Timu ya taifa na klabu.

Baada ya goli la kwanza la Lukaku, Monchengladbach waliamuka na kusawazisha bao kupitia kwa Ramy Bensebaini kwa njia ya penati baada ya Arturo Vidal kumfanyia faulo Marcus Thuram, Jonas Hofmann aliipa Monchengladbach uongozi kwa goli la pili la mchezo.

Author: Asifiwe Mbembela