Ronald Koeman akanusha taarifa kuwa ni vigumu kumfundisha Messi Barcelona

Kocha mkuu wa Barcelona Ronald Koeman amefuta tetesi zote zilizokuwa zinamhusisha staa wa kikosi chake na timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi kuwa ni vigumu kumuelekeza mshambuliaji huyo. Koeman ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mtanange wa kesho Jumatano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Dynamo Kviv katika Kundi G.

Kocha wa zamani wa Barca Quique Setien alinukuliwa akisema alipofika klabuni hapo alikuta mazingira ambayo yalikuwa yanampa ugumu kumuongoza Messi.

“Sikubaliani naye (Setien) lakini naheshimu mawazo yake kutokana na uzoefu wake, alisema Koeman aliyekuwa kocha wa Uholanzi kabla ya kupata kazi ndani ya Camp Nou.

“Kila kocha ana mbinu zake – lakini mimi nimekuwa nikizungumza nae mara kwa nara kama nahodha wangu, kiufupi tuna uhusiano mzuri” aliongeza.

Setien alifutwa kazi kufuatia Barcelona kufungwa kwa kipigo cha aibu cha goli 8-2 dhidi ya Bayern Munich Agosti 17 hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na nafasi yake kuchukuliwa na Koeman.

Author: Asifiwe Mbembela