Simba kukwaruzana na Azam fainali ya Kombe la Mapinduzi

Wekundu wa Msimbazi Simba watakabana koo na mabingwa watetezi Azam katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2019. Fainali hiyo itachezwa Jumapili Januari 14 katika uwanja wa Gombani kisiwani Pemba. Simba ilitiga fainali kupitia mikwaju ya penalti dhidi ya Malindi baada ya mechi kukamilika bila mshindi kupatikana.

Simba ilifuzu kwa mabao 3-1 ambapo waliofunga penalty hizo ni Yusuf Mlipili, Mohamed Ibrahim na Asante Kwasi huku Zana Coulibaly akipoteza tuta lake. Malindi ilifunga penalty moja tu yake Abdulswamad. Ali Juma, Muharami Issa na Cholo Ally walikosa zao.

Azam wanaelekea kutetea ubingwa wao

Hapo awali, Azam walijiweka katika nafasi nzuri ya kuhifadhi kombe hilo baada ya kuifumua KMKM mabao 3-0. Mzambia Obrey Chirwa alifikisha mabao manne katika michuano hiyo na kwa sasa ndiye anayeongoza katika ufungaji mabao.

Azam ilipata mabao yake kupitia Aggrey Morris, Salum Aboubakary na Obrey Chirwa. Kama Azam watamuangusha Simba katika fainali, basi watalihifadhi Kombe hilo kwa kuwa washindi mara tatu mfululizo.

Author: Bruce Amani