Yanga kuendelea kutafuna kiporo Kaitaba

Vita ya ligi kuu Tanzania bara kuendelea leo kwa mchezo mmoja tu, ukiwa ni mchezo kiporo kati ya Kagera Sugar dhidi ya Yanga SC. Mtanange huo utakafanyika katika dimba la Nyasi bandia, Kaitaba kuanzia majira ya saa 16:00.

Utakuwa ni mchezo namba 12 kwa upande wa Yanga ambayo ipo nafasi ya pili katika msimamo wa TPL kwa alama 29 wakati Kagera ukiwa ni mchezo namba 14.

Kuelekea mtanange huu Yanga itamkosa mchezaji mmoja Gadiel Michael aliye na maumivu kidogo ya misuli kulingana na taarifa ya Dr Bavu, maumivu aliyoyapata katika mchezo wa Jumatano dhidi ya Mwadui FC, mtanange ulioisha kwa Yanga kuibuka washindi kwa 2-1. Aidha, Tshitshimbi hatakuwa sehemu ya kikosi hicho maana aliachwa Dar es Salaam kwa sababu bado ni majeruhi.

Sambamba na hilo Yanga kwenye mchezo dhidi ya Mwadui ilimkosa Ibrahim Ajib sasa amerejea mazoezini ingawa amekuwa akilalamikiwa mara kadhaa na Kocha Mwinyi Zahera kwa utovu wa nidhamu na uvivu wakati wa mazoezi.

Kagera Sugar inashikilia nafasi ya 11 ikiwa na alama 17 baada ya michezo 13 na itahitaji ushindi kuendelea kupaa zaidi katika msimamo wa TPL.

Pamoja na mchezo huo kuwa muhimu kwa klabu zote mbili bado Kagera haina rekodi nzuri dhidi ya Yanga, mchezo wa mwisho ulipigwa katika dimba la Kaitaba, Kagera ililala 2-1

Author: Bruce Amani