Yanga yalipuliwa na Lipuli mkoani Iringa

Kikosi cha Yanga kikiwa chini ya kocha msaidizi Noel Mwandila kimeangukia pua baada ya kunyukwa goli 1-0 dhidi ya Lipuli katika mtanange uliofanyika uwanja wa Samora Mkoani Iringa ukiwa mchezo wa Ligi kuu ya kabumbu Tanzania bara.

Ukiwa mchezo wa 3 kwa Yanga kupoteza baada ya ule wa Stand United, Simba na sasa Lipuli, goli pekee la dakika ya 19 likiwekwa kimiani na Haruna Shamte kwa shuti kali kwa mpira uliotengwa na kumshinda mlinda mlango Klauis Kindoki.

Kocha mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera hajaonekana katika kikosi hicho akiwa ameenda kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Congo.

Matokeo haya yanaifanya Yanga kusalia kwenye nafasi ya kwanza ikiwa na alama zake 67 huku Lipuli wakifikisha alama 44 kwenye nafasi ya nne. Rekodi nzuri ya kupata matokeo katika uwanja huo, hivi sasa Lipuli imeivunja baada ya msimu uliopita kuvuna alama hapo.M

Mbio za ubingwa hivi sasa zimehamia katika timu tatu tu Yanga, Azam na Simba SC.

Author: Asifiwe Mbembela