Yanga yajichimbia Zanzibar kuiwinda Township Rollers Ligi ya Mabingwa

Yanga SC imefanikiwa kutua salama visiwani Zanzibar kujiwinda na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers Botswana utakaopigwa siku ya Jumamosi Agosti 10 kuanzia majira ya 12:00 jioni uwanja wa taifa Dsm.
Klabu ya Yanga imepanga kuweka kambi visiwani hapo ili kujiweka sawa kuelekea mchezo wao wa ligi ya mabingwa na Township ambapo kwenye maandalizi hayo watacheza mchezo wa kirafikii na Malindi siku ya Jumatano.
Ukiwa ni mchezo wa awali, Yanga itaingia kwenye mtanange huo ikiwa na deni kubwa kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya misimu miwili nyuma kufungwa na timu hiyo katika dimba la taifa goli 2-1 huku mafanikio ya mtani wao Simba likiwa ni deni lingine.
Akizungumza kuhusiana na kambi ya Visiwani Zanzibar kwa Yanga, Kaimu Katibu Mkuu Dismas Ten, amesema kikosi kinajichimbia huko kutokana na hilo eneo kuwa na utulivu mkubwa.
“Mchezo wetu wa kwanza nyumbani ni muhimu kushinda na tutapambana kupata matokeo, mashabiki watupe sapoti,” amesema Ten.
Kwenye safari ya Zanzibar, Yanga imeongozwa na Kocha mkuu Mwinyi Zahera, na nahodha wa kikosi hicho Papy Kabamba Tshishimbi huku wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya kitaifa wakiungana na timu hiyo Metacha Mnata, Paul Godfrey na Kelvin Yondani.

Author: Asifiwe Mbembela