Bayern yatoka nyuma mara mbili na kuibwaga Augsburg

Bayern Munich walitoka nyuma mara mbili na kuwabwaga Augsburg 3 – 2 ushindi ambao umewasaidia kupunguza mwanya kati yao na vinara Borussia Dortmund hadi pointi mbili

Leon Goretzka alijifunga katika lango lake na kuwapa wenyeji uongozi wa kushangaza baada ya sekunde 13 tu. Kingsley Coman alirejesha hali kuwa sawa muda mfupi baadaye lakini Ji Dong-won akaiweka tena Augsburg kifua mbele kwa kusukuma wavuni bao safi sana.

Coman alisawazisha tena katika muda wa mwisho wa kipindi cha kwanza, kabla ya David Alaba kukamilisha kazi na kuwapa Bayern ushindi wa pointi tatu.

Hata hivyo, kulikuwa na habari mbaya kwa Bayern, kwa sababu Coman alionekana tena kuumia katika dakika za majeruhi, kitu kilichomlazimu kuchechemea na kuondoka uwanjani.

Dortmund wanaweza kurejea mwanya wao wa uongozi kileleni kuwa pointi tano kama watawashinda Nuremberg Jumatatu usiku

Author: Bruce Amani