Dortmund waelekea mapumziko ya msimu wa baridi wakiwa kifua mbele

Borussia Dortmund imeanza mapumziko ya wiki mbili kabla ya kuanza mazoezi ya msimu wa baridi wakiwa na hisia za matumaini baada ya kuthibitisha hadhi yao ya kuwa timu inayopigiwa upatu kutwaa taji la ligi ya Bundesliga msimu huu. Dortmund iliwafunga Borussia Mönchengladbach mabao 2-1.

Dortmund iliweka rekodi ya kucheza mechi 15 bila ya kupoteza lakini hata hivyo, rekodi hiyo iliharibiwa Jumanne wiki hii baada ya kufungwa na timu ya Fortuna Düsseldorf. Dortmund itakuwa angalau na pointi sita mbele wakati ikielekea mapumziko ya majira ya baridi ingawa pia zinaweza kuwa pointi tisa kutegemea na mahasimu wao Bayern Munich ambao watashuka dimbani leo Jumamosi dhidi ya Frankfurt. Dortmund inaongoza ligi ikiwa na pointi 42 huku Bayern ikiwa nafasi ya tatu na pointi 33.

Wachezaji wa Dortmund wataelekea Marbella, Uhispania Januari 4 kwa ajili ya mazoezi ya kabla ya kuanza sehemu ya pili ya msimu, ambapo watakuwa na miadi na RB Leipzig.

Author: Bruce Amani