Dortmund warejesha mwanya wa pointi tatu kileleni

Borussia Dortmund jana iliizaba Bayer Leverkusen mabao matatu kwa mawili na kurejesha pengo la pointi tatu kileleni mwa ligi kuu ya kandanda Ujerumani – Bundesliga. Ulikuwa ushindi wao wa kwanza katika mechi nne, wakati waliwawekea breki Leverkusen ambao walikuwa wameshinda mechi nne mfululizo chini ya kocha wao mpya Peter Bosz.

Dortmund sasa wana pointi 54 huku mabingwa Bayern Munich wakiwa na 51 baada ya ushindi wao wa bao moja kwa bila dhidi ya Hertha Berlin siku ya Jumamosi. Wenyeji Dortmund walipata bao la kwanza kutoka kwa Dan-Axel Zagadou baada ya mkwaju wa kona kupigwa langoni na Raphael Guerreiro.

Kevin Volland aliwasawazishia wageni Leverkusen baada ya kazi safi na Kai Havertz, lakini dakika moja baada ya chipukizi wa Dortmund Jadon Sancho alisukuma wavuni kombora kutokana na krosi ya Abdou Diallo na kuiweka timu yake kifua mbele. Mario Gotze alifunga la tatu na kuonekana kama amefunga kazi lakini beki wa Leverkusen Jonathan Tah alifunga bao la pili kwa kichwa. Leverkusen wameanguka hadi nafasi ya saba na pointi 36.

Author: Bruce Amani