Ghana na Tunisia zabanwa katika mechi za kufuzu AFCON

Ghana na Tunisia ambazo zitakwenda kucheza Kombe la Dunia,zimetoka sare hapo jana katika mechi za kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika. Ghana ilitoka sare ya bao moja kwa moja na Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mechi ya Kundi E iliyopigwa mjini Luanda, Angola kwa sababu viwanja vya Jamhuri ya Afrika ya Kati havitoshelezi viwango vya mechi za kimataifa. Katika mechi ya pili ya kundi hilo, Angola ilitoka sare ya 1-1 na Madagascar na kujiungana Ghana kileleni mwa kundi hilo na pointi nne. Tunisia ilikabwa kwa sare tasa na Botswana jana. Katika Kundi D, Misri ilifunga bao la dakika za mwisho na kupata ushindi dhidi ya Guinea katika mechi yao ya ufunguzi mjini Cairo. Pia katika kundi D, Malawi ilipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Ethiopia mjini Lilongwe.

Author: Bruce Amani