Harambee Stars yateuliwa tuzo ya timu bora ya mwaka Afrika

TIMU ya Taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars ni miongoni mwa timu zilizoteuliwa kuwania Tuzo ya timu bora ya mwaka barani Afrika. Kenya imeteuliwa kufuatia msururu wa matokeo mazuri yakiwemo kuzifunga timu za Ghana na Ethiopia katika mchakato wa kusaka tiketi ya kushiriki michuona ya ubingwa wa Afrika mwezi Juni, mwaka ujao mjini Yaounde Cameroon.

Harambee Stars wanawania Tuzo hiyo pamoja na timu za mataifa ya Zimbabwe, Madagascar, Guinea Bissau, Mauritania na Uganda. Timu za Mali, Nigeria, Cameroon, Ghana na Afrika Kusini zimeteuliwa kuwania Tuzo hiyo katika kitengo cha wanawake.

Mshindi wa tuzo hizo atajulikana tarehe tisa mwezi Januari katika hafla itakayoandaliwa mjini Dakar, Senegal. Kura zitapigwa na makocha, waamuzi wasimamizi, mafisa wa kamati za kiufundi pamoja na manahodha kutoka mataifa 54 kote barani Afrika.

Author: Bruce Amani