Ivory Coast yainyeshea Namibia mvua ya mabao

Ivory Coast imeipa mkono wa kwa heri Namibia kwa kichapo kizito cha goli 4-1 katika mchezo wa Kimataifa Afrika Afcon uliopigwa dimba la June 30 na kuifungashia vilago timu hiyo.

Dakika ya 40 baada ya kosa kosa za hapa na pale, mshambuliaji anayekipiga Ligue 1 Ufaransa  ndani ya Toulouse Max-Alain Gradel, aliitanguliza Ivory Coast kifua mbele kabla ya mapumziko.

Kipindi cha pili dakika ya 58 Geoffroy Serey Die aliipatia timu ya I.Coast goli la pili na kufanya mchezo kuwa 2-0 kabla ya Namibia kupata goli la kufutia machozi kupitia kwa Joslin Kamatuka.

Baada ya goli la Namibia Ivory Coast iliamka na kufunga goli za haraka kupitia Wilfred Zaha na Maxwel Cornet na kuhitimisha karamu ya ushindi kwa WaIvorikosti.

Matokeo hayo yanaifanya I.Coast kufuzu moja kwa moja pamoja na Morocco kutoka kundi D wakati Afrika Kusini bado haijajua hatima yake na Namibia imeaga mashindano hayo kwa alama moja.

Author: Bruce Amani