Malawi yamzuia kigogo wa Afrika Mashariki Uganda kufuzu Afcon 2021

Timu ya Taifa ya Uganda imetupwa nje ya kuwania nafasi ya kufuzu kuingia Kombe la Mataifa Bingwa Afrika Afcon 2021 Cameroon baada ya kukubali kipigo cha goli 1-0 dhidi ya Malawi mtanange uliopigwa leo Jumatatu Machi 29 Jijini Blantyre.

Matokeo hayo yanalifanya taifa la Malawi kufuzu kuingia Kombe la Mataifa Bingwa Afrika kwa mara ya tatu tangia kuanza kwa mashindano hayo.

Bao pekee katika mechi hiyo limewekwa kimiani na mshambuliaji wa Malawi Richard Mbulu kwa kichwa na sasa wanaifikia rekodi ya mwaka 1984 na 2010.

Malawi wanaungana na timu kutoka Afrika Magharibi ya Burkina Faso kuingia kwenye fainali hizo zitakazofanyika Cameroon mwaka 2022 Januari kutoka Kundi B.

Uganda inaungana na nchi asilia katika umoja wa Afrika Mashariki za Kenya na Tanzania kutofuzu baada ya zote kutinga kwenye fainali zilizopigwa Misri.

Author: Asifiwe Mbembela