Niyonzima atua Yanga tayari kuikabili Simba Jumamosi

Winga wa kimataifa wa Rwanda Haruna Hakizimana Niyonzima amewasili Tanzania tayari kujiunga na miamba ya soka la Tanzania Yanga SC baada ya kukamilisha dili la kujiunga na timu hiyo akitokea APR ya Rwanda ambako amedumu nusu msimu baada ya kuwa Simba msimu uliopita.

Haruna Niyonzima ametua katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere Terminal 3 mchana wa leo na amepokelewa na Afisa Mhamasishaji wa Yanga Antonio Nugaz.

Niyonzima anawasili kipindi ambacho Yanga ipo katika maandalizi ya kuelekea mtanange wa Watani wa Jadi “Kariakoo Derby” dhidi ya Simba siku ya Jumamosi, Januari 4 dimba la Taifa.

Kabla ya ujio wa Niyonzima, Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli alinukuliwa akisema Haruna akiwasili nchini ataungana na wenzake moja kwa moja kwenye mazoezi ya mwisho na kama kocha atafurahishwa na kiwango chake basi anaweza akawa sehemu ya timu itakayoivaa Simba.

Kuwasili kwa Haruna kuna kamilisha idadi ya wachezaji wanne waliosaini Yanga kwenye dirisha dogo la usajili la mwezi Januari baada ya Adyum, Ditram Nchimbi, Tariq Seif Kilakala na Mivory Coast Yikpe Gilslain Gnamien

Author: Bruce Amani