Simba wapapaswa na Ruvu Shooting 1- 0 dimba la Uhuru

Ruvu Shooting imetoa adhabu nyingine kwa Simba na kutonesha kidonda cha pale wanajeshi wa magereza walipokitengeneza wiki iliyopita. Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini Tanzania wanakutana na kipigo cha pili mfululizo kwa mara ya kwanza tangu walipolichukua taji kutoka kwa Yanga baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo, walianza na Tanzania Prisons na sasa Shooting.

Bao pekee lililoipa matokeo ya alama tatu Ruvu Shooting limefungwa na mshambuliaji na nahodha wa timu hiyo Fully Maganga akitumia vyema makosa ya Pascal Wawa kunako dakika ya 35 ya mchezo ungwe ya kwanza.

Kwingineko, Azam FC imepigwa goli 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar dimba la Jamhuri ya Morogoro, Dodoma Mji FC 0-1 Tanzania Prisons. Miongoni mwa sababu za kufungwa kwa simba ni kutokuwako na wachezaji muhimu kwenye timu hiyo kama Meddie Kagere, Clatous Chota Chama na Chris Mugalu.

Author: Asifiwe Mbembela