Taifa Stars kamili gado kuwavaa Libya Afcon 2021

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inashuka dimbani leo Jumapili Machi 28 kumenyana vikali dhidi ya Libya katika mchezo wa kukamilisha ratiba ya kufuzu kuingia Kombe la Mataifa Bingwa Afrika Afcon 2021.

Taifa Stars ambayo inanolewa na kocha Kim Poulsen iliangukia pua kwenye mechi iliyopita dhidi ya Equatorial Guinea kwa kupoteza bao 1-0 hivyo itakuwa inahitaji ushindi kuwafuta machozi Tanzania kwani hata ikishinda haitaweza kufuzu kuingia kwenye fainali hizo.

Stars ikiwa ipo kundi J ina pointi zake nne baada ya kucheza mechi tano. Inakutana na Libya ambayo ipo nafasi ya nne na ina pointi tatu baada ya kucheza mechi tano.

Kim Poulsen, Kocha Mkuu wa Stars amesema kuwa wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mchezo wao huo na wana amini watapata ushindi.

“Kupoteza mchezo wetu uliopita ni somo kwani hatukuhitaji kupoteza kwa kuwa imetokea basi tunajipanga kwa ajili ya mchezo wetu ujao,” .

Poulsen amerithi mikoba ya Etiene Ndayiragije ambaye alifutwa kazi kwa makubaliano kati yake na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) ambaye pia alichukua mikoba ya Emmanuel Amunike raia wa Nigeria.

Author: Asifiwe Mbembela