Taifa Stars yapoteza nafasi ya kucheza Afcon, yachapwa 1-0 na Equatorial Guinea

Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars imepoteza mchezo wake wa makundi kuwania nafasi ya kucheza michuano ya Kombe la Mataifa Bingwa Afrika – Afcon mwaka 2022 nchini Cameroon dhidi ya Equatorial Guinea kwa bao 1-0 mtanange uliopigwa leo Alhamis Machi 25.

Tanzania yenye alama nne walikuwa wanahitaji ushindi kufufua matumaini ya kufuzu kwa mara ya pili katika mashindano hayo makubwa ngazi ya taifa lakini sasa wameipa uhakika Equatorial Guinea kufuzu baada ya kufikisha alama tisa.
Bao pekee limefungwa na Emilio Nsue dakika za mwishoni kabisa mwa ungwe ya pili.
Hata hivyo, Tanzania itakamilisha ratiba dhidi ya Libya katika uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam mtanange utakaokuwa kwa ajili ya kukamilisha tu ratiba kwani alama ilizonazo Tunisia (13) na Equatorial Guinea (9), Tanzania (4) na Libya (3) haziwezwi kufikiwa.
Ikiwa chini ya kocha mpya Kim Poulsen baada ya kufutwa kazi kwa Ettiene Ndayaragije, Stars imefurukuta lakini wapi walikuwa wenyeji ambao walikosa goli nyingi kabla ya kujipatia goli hilo moja na la ushindi.

Author: Asifiwe Mbembela