Tunisia yaiondoa Ghana kwa mikwaju ya penalti

Katika dimba la Ismailia nchini Misri umechezwa mtanange wa kukatana na shoka kati ya Ghana dhidi ya Tunisia mashindano ya Afcon 2019 mchezo uliomalizika kwa Tunisia kusonga mbele kwa penati 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare 1-1.
Ghana ikiwa ni miongoni mwa timu zilizopewa nafasi ya kufanya vizuri katika mashindano ya mwaka huu ilijikuta ikiwa nyuma ya goli moja la Taha Yassine Khenissi katika dakika za mwanzo za kipindi cha pili kabla ya Ghana kusawazisha kupitia goli la kujifunga la Rami Bedoui kunako dakika za lala salama.
Baada ya dakika tisini, refarii akaongeza dakika 30 ambazo bado hazikufanya mbao za matokeo kubadilika mpaka matuta ndiyo yaliyoamua mchezo huo kwenda katika faida ya Tunisia.
Mshambuliaji wa Leeds Caleb Ekuban ndiye mchezaji pekee aliyekosa penati kwa upande wa Ghana na kwa mchezo mzima.
Hii inakuwa mara ya tatu kwa Ghana kuondolewa katika mashindano rasmi kwa njia ya matuta baada ya kuondolewa na Uruguay Kombe la Dunia mwaka 2010, Ivory Coast mwaka Afcon 2017 na sasa tena 2019 dhidi ya Tunisia.
Black Stars wanaungana na Misri, Morocco na Congo kwa Mataifa makubwa kuondolewa mapema kwenye michuano ya Afcon mwaka 2019 nchini Misri.

Author: Bruce Amani