Ujerumani yalenga kujinyanyua baada ya Kombe la Dunia

Ujerumani wanaanza upya kufuatia janga lililowakumba katika Kombe la Dunia, kwa kibarua kikali dhidi ya mabingwa wapya wa dunia Ufaransa siku ya Alhamisi. Mchuano huo wa Ligi ya Mataifa ya Ulaya – UEFA Nations League unatoa fursa ya kuchukua hatua ya kwanza kuelekea kutwaa taji jipya.

Uholanzi pia ipo katika Kundi la kwanza kati ya manne ya ngazi ya juu ya League A, ambapo washindi wa makundi watafuzu katika fainali za dimba hilo mwaka ujao. Mlinda mlango wa Ujerumani Manuel Neuer anasema ni wakati wa kusahau yaliyopita na kuganga yajayo “tunawajibika kwa kujiwekea shinikizo sisi wenyewe, lakini tunaisburi kwa hamu michezo ijayo na tuna furaha kuwa tutacheza dhidi ya timu nzuri sana, Ufaransa ambao ndio mabingwa wa dunia. Kutakuwa na mabadiliko kadhaa kikosini. kikosi kinaonekana tofauti kidogo na pia viongozi wapya.  Sote tunasubiri kuona na bila shaka tunataka kuwa sehemu ya kuleta tena mafanikio” Asema Neuer.

Ligi Ya Mataifa ilianzishwa kutokana na wazo la rais wa zamani wa Shirikisho la Kandanda Ulaya – UEFA Michel Platini, ambaye alitaka kuyapa mataifa madogo ya mashariki mwa Ulaya mapato ya kutosha kutoka kwa mauzo ya pamoja ya kinyang’anyiro kipya.

Author: Bruce Amani