Harambee Stars waondoka katika mbio za kuwania kufuzu Afcon kwa ushindi wa 2-1 ugenini dhidi ya Togo

Harambee Stars wamemaliza kampeni yao ya kuingia kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa heshima baada ya kuwalaza Togo 2-1 na kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Kundi G.

Mechi ya Jumatatu, Machi 29, ndiyo ilikuwa ya mwisho ya makundi lakini haikuwa na uzito wowote kwa timu zote mbili.

Stars walizuru Togo baada ya droo ya 1-1 dhidi ya Misri waliopata kwenye mechi iliyoandaliwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Kasarani mjini Nairobi.

Ushindi katika mechi hiyo ungeyaweka hai matumaini yao ya kufuzu katika fainali za AFCON ambazo zimeratibiwa kuandaliwa Cameroon 2022.

Lakini hayo hayakuwazuia vijana wa kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee kurekodi matokeo mazuri ugenini huku Hassan Abdallah akionja wavu wa Sparrowhawks.

Staa huyo wa Bandari alifungua ukurasa wa mabao punde baada ya muda wa mapumziko kabla ya Masud Juma kusawazisha katika dakika ya 65.

Juhudi za wenyeji kupata bao la kufutia machozi zilizaa matunda kupitia kwa Henri Eninful ambaye alifanya mambo kuwa 2-1.

Licha ya matokeo hayo ya kuridhisha ugenini, Stars hawataingia kwenye fainali ya AFCON huku Comoros na Misri wakifuzu.

Author: Bruce Amani