Taifa Stars yashinda 1-0 kwa Libya, yatupwa nje ya Afcon 2021 Cameroon

Taifa Stars leo Machi 28 imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Libya kwenye mchezo wa kuwania kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Mataifa Bingwa Afrika, (Afcon) uliochezwa Uwanja wa Mkapa Jijini Dsm.Bao pekee la ushindi kwa Stars lilipachikwa kimiani na Simon Msuva kunako dakika ya 45 kwa kichwa akiwa ndani ya 18.

Bao hilo lilidumu mpaka dakika 90 licha ya kipindi cha pili Libya kufanya mashambulizi makali matatu yaliokolewa na kipa Aishi Manula huku Stars wakiwa na kazi ya kulinda lango katika dakika za lala salama kwa kuwa wapinzani wao waliwaandama mwanzo mwisho.

Licha ya Stars kushinda imeongeza pointi zake tatu na kufikisha jumla ya pointi 7 ndani ya kundi J ila haina nafasi ya kufuzu Afcon kwa kuwa tayari Tunisia inayoongoza kundi ikiwa na pointi 16 na Equatorial Guinea yenye pointi 9 zimeshakata tiketi ya kwenda Cameroon wakati timu ya Libya imeshika mkia ikiwa ina alama tatu.

Author: Asifiwe Mbembela