Mbappe aipa PSG ushindi mnono

Kylian Mbappe alifunga mabao manne katika dakika 13 wakati Paris Saint Germain iliendeleza uongozi wake kileleni wa ligi kuu ya kandanda ya Ufaransa na pengo la point inane kwa kuirarua Lyon 5-0. Mbappe alifunga manne katika kipindi cha pili yakiwemo matatu katika dakika nane na kufikisha 10 idadi ya mabao aliyofunga msimu huu mpaka sasa.

PSG imeendeleza rekodi  yake ya asilimia 100 kwa kushinda mechi zake zote tisa za ligi .

Timu zote zilimaliza mchezo na wachezaji kumi uwanjani baada ya Lucas Tousart kuonyeshwa kadi nyekundu kwa upande wa Lyon baada ya Presnel Kimpembe kutimuliwa kwa upande wa wenyeji.

Monaco bado haijapata ushindi mpaka sasa tangu msimu kuanza baada ya Rennes kupata ushindi wa 2-1 katika uwanja wa Stade Louis II

Marseille iliichabanga Caen 2-0 uwanjani Stade Velodrome kutokana na mabao ya Kostas Mitroglou na Florian Thauvin, ambalo ni la saba la mshambuliaji huyo msimu huu.

Marseille sasa imesonga hadi nafasi ya tatu, kufuatia ushindi wa PSG, wako nyuma ya viongozi hao na pengo la pointi 11.

Bordeaux ilisonga hadi nafasi ya saba baada ya kupata ushindi rahisi wa 3-0 dhidi ya Nantes.

Author: Bruce Amani