Ronaldo na Juve waendelea kuitikisa ligi kuu ya Italia

Vinara wa Ligi kuu ya kandanda Italia Juventus wameutanua uongozi wao kileleni na pengo la pointi 11 baada ya kuibwaga Fiorentina Jumamosi.

Mabingwa hao walichukua uongozi kupitia kombora kali la mita 18 kutoka kwa Rodrigo Bentancur baada ya kugongeana pasi na Paulo Dybala.

Giorgio Chiellini akafunga bao lake la kwanza baada ya miezi 18. Kisha Cristiano Ronaldo akafunga bao lake la 10 katika Serie A kupitia penalty baada ya mchezaji wa Fiorentina kuunawa mpira.

CR7 ambaye alinunuliwa na Juve kwa kitita cha pauni milioni 99 kutoka Real Madrid sasa amemfikia Krzysztof Piatek wa Genoa katika msimamo wa mfungaji bora nchini Italia. Juve wameshinda 13 kati ya mechi 14 walizocheza msimu huu. Na wanawinda taji lao la nane mfululizo la Serie A. Napoli ambao wanashikilia nafasi ya pili kwenye ligi watacheza dhidi ya Atalanta Jumatatu.

Author: Bruce Amani