Senegal kupepetana na Tunisia nusu fainali

Usiku wa dei haukawii kufika katu. Baada ya mapumziko ya siku mbili, leo hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika Afcon 2019 kuendelea tena ambapo Senegal ataikaribisha Tunisia.

Katika majira ya 1 usiku, Simba wa Teranga Senegal ikiwa inapewa nafasi ya kuwa mabingwa inaikaribisha Tunisia nusu fainali katika dimba la June 30.

Senegal tangu mwanzo wa michuano hii imepoteza mchezo mmoja tu ule wa Algeria hatua ya makundi huku awamu ya robo fainali ikiitoa Benin kwa goli 1-0.

Tunisia haijapoteza hata mchezo mmoja kuanzia hatua ya makundi  ilikuwa haipewi nafasi ya kufanya vizuri lakini tangu imeiondosha Madagascar kwa goli 3-0 robo fainali na jinsi walivyocheza kitimu, matumaini ya kufanya vizuri yamerejea kwao.

Timu hizi zinakutana zikiwa na aina mbili tofauti kiuchezaji. Senegal imekuwa ikifanya vizuri kutokana na ubora wa kikosi chake licha ya kutokuwa na muunganiko mzuri kiuchezaji. Wakati Tunisia inacheza kitimu zaidi kwa kutomtegemea staa yeyote jambo linaloonekana linatoa matunda mazuri mpaka sasa

Author: Asifiwe Mbembela