Yanga yaibwaga Alliance na kutinga nusu fainali Kombe la FA

Yanga imesonga mbele hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania baada ya kuifunga Alliance FC kwa mikwaju ya penati baada ya dakika 90 za mwamuzi kumalizika kwa sare 1-1.

Mtanange ukiwa wa tatu ndani ya msimu mmoja, ulikuwa wa piga nikupige kwa dakika zote 90 za mwamuzi Zabroni. Timu zote zimetengeneza nafasi za wazi za kufunga lakini umakini wa washambuliaji ulikuwa kikwazo.

Goli la Yanga limefungwa na Heritier Makambo kwa shuti kali dakika ya 38 lililozua utata kama limeingia au hapana huku lile la kusawazisha likifungwa na Joseph James dakika ya 61 kwa kichwa.

Baada ya matokeo hayo Yanga imekamilisha timu nne zilizoingia hatua ya nusu fainali baada ya Lipuli FC ya Iringa, Kinondoni Municipal  Council ya Dar es Salaam na Azam ya DSM.

Hatua ya nusu fainali itazikutanisha Lipuli FC dhidi ya Yanga katika uwanja wa Samora Iringa wakati mchezo mwingine utafanyika dimba la Uhuru ambapo KMC itakuwa mwenyeji wa Azam FC.

Mshindi wa mashindano haya anaiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambapo msimu uliopita Mtibwa Sugar iliiwakilisha nchi huko ingawa ilishatolewa tayari kwenye hatua za mwanzo.

Azam pamoja na Yanga ndio timu pekee zilizowai kutwaa ubingwa wa Kombe hili kwa nyakati tofauti.

Matokeo mengine robo fainali

-Lipuli FC 2-0 Singida United

-KMC 2-0 African Lyon

-Kagera Sugar 0-1 Azam FC

Author: Asifiwe Mbembela