Yanga na Township Rollers nguvu sawa Dar es Salaam

Yanga imetosha nguvu kwa kutoa sare ya goli 1-1 na Township Rollers ya Botswana katika mchezo wa Ligi ya mabingwa Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam hatua ya awali ya michuano hiyo.
Yanga ikiwa na muonekano mpya wa kikosi kulinganisha na msimu uliopita (2018/2019) imeonyesha kandanda safi ikisaidiwa na takwimu katika uwiano wa kona, umiriki wa mpira na mipira iliyolenga goli pamoja yote hayo ilishindwa kupata goli.
Katika dakika 45 za kwanza Yanga ilitengeneza mashambulizi mengi licha ya kushindwa. Katika dakika hizo kiungo mshambuliaji wa timu Patrick Sibomana alikosa penati 38′ baada ya mlinzi wa Rollers kuunawa mpira ndani ya 18.
Wakati Yanga ikitafuta goli kwa nguvu ilijikuta ikifungwa goli la kushitukiza baada ya shambulizi la haraka lililofungwa kwa shuti kali nje kidogo ya kumi na nane na Phenyo Seremeg kunako dakika 7.
Iliwachukua mpaka kipindi cha pili dakika ya 87 Yanga kusawazisha goli kwa penati baada ya Township Rollers kunawa mpira tena ambapo safari hii Sibomana alijikosoa na kufunga penati nzuri.
Yanga itasafiri kwenda Botswana baada ya wiki moja katika mchezo wa marejeano.
Kikosi cha Yanga kilichoanza ni Metacha Mnata, Paul Godfrey (Ali Ali), Muharami Issa Marcello, Ally Sonso Mtoni, Lamine Moro, Papy Kabamba Tshishimbi, Mohammed Issa Banka, Mapinduzi Balama(Mrisho Ngassa), Juma Balinya(Issa Bigirimani), Sadney Ukirhrob na Patrick Sibomana.

Author: Asifiwe Mbembela