Chelsea Yaichapa Lille 2-0 Ligi ya Mabingwa Ulaya

Chelsea imeibuka na ushindi wa goli 2-0 dhidi ya Lille katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora mchezo uliopigwa dimba la Stamford Bridge Jumanne ya Februari 21.

Ushindi huo unawapa nafasi kubwa ya kufuzu kucheza robo fainali ingawa watalazimika kutunza ushindi huo kwenye mechi ya marejeano.

Mabao ya Kai Havertz na Christian Pulisic yalitosha kabisa kuwapa uhakika wa ushindi, Havertz alifunga akimalizia mpira wa kona wa Hakim Ziyech wakati Pulisic ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Marekani akifunga kwa pasi ya NG’olo Kante.

Kwenye mechi hiyo, baada ya kupokea ukosoaji mkubwa mshambuliaji Romelu Lukaku hakuanzishwa na badala yake alitumiwa kiungo mshambuliaji Havertz ambaye alikuwa kwenye ubora.

Hata hivyo, maumivu kwa Chelsea ya Thomas Tuchel ni kuumia kwa kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Croatia Mateo Kovacic na winga wa Morocco Hakim Ziyech kuelekea mtanange wa Jumapili dhidi ya Liverpool dimba la Wembley fainali ya kombe la Carabao.

Author: Asifiwe Mbembela