Juventus yaendeleza ubabe katika ligi ya Italia

Kuna msemo maarufu unaosema kuwa katika Ligi ya Italia, unapotaja Juventus, bila kujali mambo yatakuwaje, au itaavyocheza, Juve kila mara hupata tu mbinu ya kushinda. Hili lilikuwa wazi katika mechi ya jana ya Derby della Mole, ambapo mabingwa hao wa Italia walikuwa wa kiwango cha chini kabisa lakini wakamudu kujikusanyia pointi tatu.

 

Baada ya kuzabwa na Young Boys katikati ya wiki katika Champions League, Juve walitaka kurejea katika hali yake bora lakini ni wazi kuwa walidhibitiwa na kusumbuliwa na Torino, ambao wako katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi.

 

Il Toro ilicheza kwa nidhamu kubwa na kumudu kuwanyamazisha kabisa nyota wa Juve kwa sababu Cristiano Ronaldo, Mario Mandzukic na Paulo Dybala walishindwa kutamba kabisa dhidi ya mahasimu wao.

 

Lakini mwishowe penalty aliyofunga CR7 ilitosha kuhakikisha kuwa Juve wanapata ushindi wa 1-0 na kuendeleza rekodi yao ya kutoshindwa mechi msimu huu katika Serie A.

 

Ronaldo alifunga bao lake la 11 la ligi kupitia penalty baada ya kipa wa akiba Salvador Ichazo kumuangusha Mandzukic kwenye eneo la hatari. Juve sasa imejikusanyia pointi 46 kati ya 28 ambazo wangeweza kupata katika mechi 16.

Katika matokeo mengine ya mechi za Jumamosi, Inter Milan ilijiimarisha katika nafasi ya tatu baada ya kuishinda Udinese 1-0.

Author: Bruce Amani