Kocha wa Yanga Kaze akubali kipigo cha Coastal Union, asema macho mbele

Kocha mkuu wa Yanga, Cedric Kaze amesema anakubaliana na matokeo ya kupoteza ya mchezo wa Jana Alhamis dhidi ya Coastal Union na sasa wanaenda kujipanga kwa ajili ya michezo iliyo mbele yao.

Jana Machi 4, kikosi cha Coastal Union kiliibuka na ushindi wa bao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Tanzania VPL na klabu hiyo ya kocha Juma Mgunda inakuwa ya kwanza kuifunga Yanga msimu huu.

Akizungumzia mchezo huo kocha Kaze amesema hana wa kumlaumu kwani refarii amechezesha vizuri kabisa.

Kaze amesema “tulikuwa na mchezo mzuri dhidi ya wapinzani wetu na kufanikiwa kupata penalti mwanzoni, lakini kwa bahati mbaya tuliikosa.

“Lakini nawapongeza vijana wangu kwa kupambana, pamoja na wapinzani wetu kwa ushindi walioupata”.

Yanga watashuka tena dimbani siku ya Jumapili kucheza dhidi ya Polisi Tanzania Mtanage wa VPL.

Author: Asifiwe Mbembela