Polisi kuchunguza madai ya ubakaji dhidi ya Ronaldo

Polisi imesema imeanzisha upya uchunguzi wa madai ya ubakaji dhidi ya Cristiano Ronaldo. Mawakili wa nyota huyo wa kandanda wanatishia kulishtaki jarida la Ujerumani baada ya kuchapisha ripoti ya madai hayo.

Cristiano Ronaldo anashitakiwa nchini Marekani na mwanamke anayedai kuwa nyota huyo Mreno alimbaka mwaka wa 2009.

Raia huyo wa Marekani Kathryn Mayorga anasema Mreno huyo alimbaka mara kadhaa katika hoteli walimokuwa mjini Las Vegas wakati akipiga mayowe ya kujaribu kumkataza, kwa mujibu wa kesi iliyowasilishwa Ijumaa katika Kaunti ya Clark, Nevada.

CR7 anakanusha madai hayo akiyaita “habari bandia”. Mawakili wa nyota huyo wa Juventus wamesema Ijumaa kuwa watalishtaki jarida la Der Spiegel la Ujerumani baada ya awali kuchapisha madai ya Mayorga. Polisi ya Las Vegas imethibitiha kuwa inachunguza madai hayo.

Mshindi huyo mara tano wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka anakanusha madai hayo, akisisitiza kuwa kitendo hicho cha ngono kilikuwa cha maelewano.

Nyota huyo wa Juventus hajatoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo lakini Jumapili alionekana kwenye video Instagram live.

“Habari bandia, waataka kujipa sifa kwa kutumia jina langu. Ni kawaida,” alisema. “wanataka kuwa maarufu kwa kusema jina langu. Lakini kama ni sehemu ya kazi hiyo, mimi ni mwanamme mwenye furaha na kila kitu kiko sawa.”

Author: Bruce Amani

JuventusRonaldo