Juventus yabeba ubingwa wa Italia mara ya nane mfululizo

Ameshinda katika ligi kuu ya England, akashinda katika ligi kuu ya Uhispania, na sasa ameshinda katika ligi kuu ya Italia.

Cristiano Ronaldo amesema atabaki Juventus kwa asilimia 1,000 baada ya klabu hiyo kubeba ubingwa wa ligi kuu ya Italia kwa msimu wa nane mfululizo.

Vijana hao wa Massimiliano Allegri Juve waliwabwaga Fiorentina 2 – 1 katika mechi ya ligi leo Jumamosi. Walijikuta bao moja nyuma kupitia Nikola Milenkovic aliyewafungia wageni Fiorentina kabla ya Alex Sandro kusawazisha kwa kichwa safi katika dakika ya 37.

Ushindi wao ulikamilika katika kipindi cha pili wakati German Pezzella alipojifunga katika lango lake mpira uliopigwa na Ronaldo.

“Nina furaha sana kwa sababu nimeshinda taji la Italia katika msimu wangu wa kwanza,” alisema Ronaldo.

“Bila shaka, mambo hayakwenda vizuri katika Champions League, lakini tutarudi tena mwaka ujao.”

Author: Bruce Amani