Baleke, Oliviera Watamba Ligi Kuu

266

Mshambuliaji wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Jean Baleke amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Machi wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2022/23, huku Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Roberto Oliviera, akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Kikao cha Kamati ya Tuzo za TFF kilichokutana Dar es Salaam leo Jumamosi Aprili 8, 2023, kimemchagua Baleke, baada ya kuonesha kiwango kizuri kwa mwezi Machi na kutoa mchango mkubwa kwa Simba, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu katika dakika 81 alizocheza, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 ugenini.

Baleke aliwashinda Daruweshi Saliboko wa KMC na Jeremiah Juma wa Tanzania Prisons alioingia nao hatua ya fainali. Kwa mwezi Machi kila timu ilicheza mchezo mmoja tu.

Kwa upande wa Oliviera aliwashinda Nasreddine Nabi wa Yanga na Abdallah Mohammed wa Tanzania Prisons katika hatua ya fainali, ambapo kwa mwezi huo Simba ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Author: Asifiwe Mbembela