Denmark waichapa Czech watinga nusu fainali Euro 2020 kuchuana vikali na England

195

Denmark licha ya kukumbwa na tukio la kihisia ambalo pengine ungefikiri lingewaharibu kiakili lakini wapi wameendelea kusonga hata katika vigingi vizito vya Euro 2020 kufuatia kutinga hatua ya nusu fainali mbele ya Jamhuri ya Czech Jana Jumamosi Julai 3.

Itakumbukwa mwanzoni mwa michuano hiyo, Denmark walimpoteza kiungo mshambuliaji wao anayekipiga kunako klabu ya Inter Milan Christian Eriksen kufuatia kupoteza fahamu uwanjani katika mchezo dhidi ya Finland.

Walianza kwa kipigo cha Finland, hawakukata tamaa, hatua ya 16 bora wakamchapa Wales na kukutana na Czech ambaye pia wakatoa kichapo cha goli 2-1.

Bao la kwanza likiwekwa kimiani na Thomas Delaney huku kasi ya mashambulizi kwenye goli la Czech yakiendelea kisha wakapata bao la pili kupitia kwa Kasper Dolberg akimalizia krosi ya Joakim Maehle.

Jamhuri ya Czech walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Patrik Schick ambaye sasa anafikisha goli tano sawa na nyota wa Juventus na Ureno Cristiano Ronaldo katika mbio za kiatu cha dhahabu.

Denmark watacheza na England Jumatano Julai 7 dimba la Wembley kukiwa na mashabiki asilimia 75 ya uwezo wa uwanja.

Author: Asifiwe Mbembela