Miaka 55 ya England yafuzu fainali ya michuano mikubwa Ulaya, kuchuana vikali na Italia Euro 2020

245

England imefanikiwa kuibuka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya Denmark katika mchezo wa Euro 2020 hatua ya nusu fainali mtanange uliopigwa dimba la Wembley Jana Jumatano huku wakivunja rekodi ya kukosa fainali kubwa kwa takribani miaka 55.

Mara ya mwisho kwa England kufika fainali ya michuano na mashindano mbalimbali ya kimataifa ilikuwa mwaka 1966 kipindi ambacho waliishinda Ujerumani Magharibi fainali ya Kombe la Dunia.

Mbele ya mashabiki takribani 66,000 England walinyamazishwa na bao la mkwaju wa freekick wa nyota wa Denmark Mikkel Damsgaard hatua 30.

Hata hivyo, Denmark walipoteza kujiamini na kujikuta wanajifunga kupitia kwa nahodha Simon Kjaer akishindwa kuokoa vyema krosi ya winga wa Arsenal Bukayo Saka.

Kipa wa Leicester City na Denmark Kasper Schmeichel alikuwa kwenye mchezo mzuri kufuatia kufanya sevu nzuri za Harry Maguire na Harry Kane ingawa katika muda wa ziada dakika ya 104, Kane aliingia kambani na kumaliza mtanange huo.

Goli la Kane likiwa ni mkwaju wa penati kufuatia winga Raheem Sterling kufanyiwa faulo na Joakim Maehle.

Kane anafikisha bao 10 sawa na lijendi Gary Lineker katika mashindano makubwa.

Baada ya kufuzu kuingia hatua ya fainali ya Euro 2020, England itapepetana vikali na Italia katika mechi ya fainali itakayopigwa dimba la Wembley Jumapili Julai 11.

Author: Asifiwe Mbembela