Sarpong, Onyango watoa pointi moja moja Yanga, Simba VPL

479

Kariakoo Derby yamalizika kwa sare, wababe wa Jiji la Dar es Salaam wagawana alama, kufuatia sare ya 1-1 mtanange uliopigwa dimba la Benjamin Mkapa Novemba 7.

Yanga wakiwa wa kwanza kupata goli kupitia kwa Michael Sarpong kwa njia ya penati kufuatia beki Joash Onyango kumfanyia faulo winga teleza Tuisila Kisinda ungwe ya kwanza.

Likiwa ni bao lake la tatu kwenye mbio za Ligi Kuu nchini Tanzania baada ya kuwafunga Tanzania Prisons, Biashara United na sasa Simba, lakini pia ikiwa mechi yake ya kwanza ya dabi.

Kwa upande wa Simba ungwe ya kwanza unaweza sema ilikuwa ya Yanga wakati ambao Simba ilicheza vizuri kipindi cha pili hasa mabadiliko ya kuingia kwa Hassan Dilunga aliyeongeza kasi ya mchezo.

Bao la Simba limewekwa kimiani na mlinzi Onyango ni kama alikuwa anafuta makosa yake ambapo lilitokana na mpira wa kichwa wa Luis Miqussone dakika ya 86.

Matokeo hayo yako chanya kwa pande mbili kwa sababu endapo Yanga ingeshinda ilikuwa inaenda kutengeneza mwanya wa alama sita ambapo sare hiyo angalau imebakiza pengo la alama nne timu zote zikiwa na michezo 10.

Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 20, wakati huo huo Yanga ina pointi 24 na Azam FC alama 25 baada ya mechi 10 za mwanzo kwa timu zote.

Author: Asifiwe Mbembela