Simba yainyuka Power Dynamo katika kilele cha Simba Day

373
Simba imefanikiwa kupata ushindi wa goli 3-1 dhidi ya Power Dynamo ya Zambia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam katika kuhitimisha Kilele cha Simba Day.
Ikiwa ni mwaka wa 10 tangu kuanza maadhimisho ya Simba Day, siku ya leo ilifanikiwa kuujaza Uwanja wa taifa (60,000) huku wakitambulisha wachezaji wao wapya akiwemo kipenzi Ibrahim Ajibu.
Ushindi wa Simba ulianza kuandikwa katika dakika za mapema kipindi cha kwanza 3′ baada ya “Terminator” Meddie Kagere kuandika bao la kuongoza kupitia uzembe wa mlinda mlango
Kunako dakika ya 58 Meddie Kagere akaandika bao la pili akimalizia pasi ya winga raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Deo Kanda.
Furaha ya Simba kwa Wanasimba ikazidi maradufu kupitia goli la mwisho la Mnyarwanda huyo aliyezaliwa Uganda Medie Kagere dakika ya 77
Kwa upande wa Power Dynamo wao walifunga bao dakika ya 24 kupitia kwa Jimmy baada ya mabeki wa Simba kujichanganya katika mpira wa kona uliopigwa kuelekea kwenye kona yao.
Kiujumla mchezo ulikuwa mzuri wenye kuvutia hasa katika eneo la katikati la uwanja ambapo eneo hilo lilitawaliwa na viungo wanne, Clatous Chota Chama, Mzamiru Yasni, Shibobo na Francis Kahata.
Hata hivyo, Simba itajilaumu yenyewe kwa kukosa nafasi wazi kadhaa licha ya kuwakosa wachezaji kadhaa  wenye shabaha na goli kama Ibrahim Ajibu, John Bocco na Mkude Jonas.

Author: Asifiwe Mbembela