Simba yatafuna kiporo cha JKT Tanzania, yawafunga 3-0

308

Klabu ya Simba imefanikiwa kuondoka na alama tatu katika mchezo wa kiporo dhidi ya JKT Tanzania mtanange wa Ligi Kuu nchini Tanzania VPL uliopigwa Leo Jumatatu Machi 1 katika dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Simba ambayo inakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa VPL, imeshinda 3-0 na kufikisha pointi 45 ikibakia katika nafasi hiyo ingawa inanufaika na kuwa na michezo miwili mkononi.

Wakiwa kwenye utawala bora wa mchezo na katika kiwango kizuri msimu huu Simba ilijipatia magoli yake kupitia kwa Cris Mugalu ambaye alitupia bao la kwanza akimalizia krosi ya Luis Miquissone kabla ya Luis Miquissone mwenyewe kuongeza bao la pili dakika chache kabla ya mapumziko akitumia vyema pasi ya kiraka Erasto Nyoni.

JKT Tanzania iliyo chini ya Abdallah Mohammed Balesi ilirudi vyema ungwe ya pili na kupunguza makosa kwa kiasi fulani kulikochagizwa na maingizo mapya lakini dakika za lala salama nahodha John Raphael Bocco alikwamisha mpira nyavuni kwa kumalizia mpira wa Larry Bwalya na kufanya jumla ya goli 3-0.

Baada ya mchezo huo, Simba watakuwa na safari kuelekea nchini Sudan kumenyana na Al Merreikh mchezo wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Simba wakiwa vinara wa kundi lao ambalo lipo na timu ya AS Vita, Al Ahly na Merreikh.

Author: Asifiwe Mbembela