Yanga yaifumua Tanzania Prisons 2-1

645

Vinara wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara klabu ya Yanga imeibuka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya wenyeji Tanzania Prisons kwenye mtanange uliopigwa dimba la Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Ushindi huo wameupata Leo Jumapili Disemba 19, 2021 ambapo kabla ya kuanza kwake kulikuwa na taarifa kuwa huenda ukaahirishwa kutokana na baadhi ya wachezaji kutajwa kuwa ni wagonjwa hata hivyo umepigwa.

Prisons ambao wamekuwa wakisifika kwa matumizi ya nguvu, walikuwa wa kwanza kuandikisha bao kupitia kwa Samson Mbangula aliyemalizia mpira wa kona kunako dakika ya 13 ya mchezo ikiwa ni pigo lao la kwanza pia.

Yanga walijibu mapigo kwa kufunga goli kupitia kiungo mshambuliaji Feisal Salum “Fei Toto” akimalizia mpira wa kichwa wa Khalid Aucho na baadaye goli la ushindi likifungwa na Khalid kwa kichwa akifunga bao hilo kupitia krosi maridhawa ya kiungo Saido Ntibanzokiza.

Ushindi huo unaifanya Timu ya Wananchi Yanga kufikisha alama 23 kileleni mwa msimamo wa Ligi, alama tano zaidi ya Simba iliyonafasi ya pili na Prisons wanasalia nafasi ya 13 na alama 8.

Author: Asifiwe Mbembela