Bodi ya Ligi Tanzania yatoa ushauri kwa vilabu

303

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imezishauri klabu zote kutumia vema kipindi hiki cha mapumziko ya Ligi kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi, kwa kuwekeza nguvu katika kuboresha miundombinu ya viwanja vyao vinavyotumika kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2021/2022.

Hii ni baada ya Bodi kukutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Leseni za Klabu na kukubaliana juu ya mkakati wa maboresho ya viwanja ili Ligi itakaporejea viwe katika hali nzuri zaidi.

Ubora wa viwanja ni katika masuala muhimu yaliyoainishwa kwenye masharti ya Leseni za Klabu (Club Licensing Regulations) ambapo Bodi
ya Ligi inazikumbusha klabu zote kuwa masharti hayo yanatekelezwa kwa asilimia 100 kuanzia msimu huu wa 2021/2022.

Bodi ya Ligi inazikumbusha klabu kufanya marekebisho/maboresho ya
viwanja vyao katika maeneo yote muhimu hasa;
1. Eneo la kuchezea (Pitch)
2. Vyumba vya kuvalia (Dressing Rooms)
3. Uzio wa kutenganisha eneo la kuchezea na washabiki.

4. Maeneo ya kukaa wachezaji wa akiba na viongozi wa benchi la
ufundi wakati wa mchezo (Technical Area/Benches), na
5. Vyoo vya washabiki

Kamati ya Leseni za Klabu itakagua viwanja vyote kabla ya mechi za mzunguko wa 12 ambazo zitachezwa Januari 14, 2022 na vile

vitakavyokosa sifa za kikanuni na sheria havitaruhusiwa kutumika.

Author: Asifiwe Mbembela