Denmark yatinga robo fainali Euro 2020 yaichapa Wales 4-0

204

Wales imetolewa rasmi kwenye michuano ya Euro 2020 baada ya kukubali kipigo cha goli 4-0 kutoka kwa Denmark katika mchezo wa 16 bora uliopigwa Leo Jumamosi wakati ambao Denmark wanaingia kwenye robo fainali ya michuano hiyo.

Denmark ambao baada ya tukio la kupoteza fahamu uwanjani kwa kiungo mshambuliaji wa Inter Milan Christian Eriksen hakuna aliyedhania wangerudi katika ubora mkubwa walianza kupata goli kupitia kwa Kasper Dolberg kunako dakika ya 27 kabla ya Dolberg kuongeza bao la pili dakika ya 47 kufutia makosa ya Neco Williams.

Wales waliokuwa wanapata shida hata katika hatua ya makundi kama Denmark waliendelea kupoteana uwanjani ambao walifungwa goli la tatu na Joakim Maehle.

Akiingia kutokea bechi Harry Wilson alionyeshwa kadi nyekundu na baadaye mshambuliaji wa Barcelona Martin Braithwaite akaingia kambani kwa bao la nne la mchezo.

Ushindi huo kwa Denmark unaifanya kufuzu kuingia hatua ya robo fainali ya Euro 2020 ambapo itacheza na mshindi kati ya Jamhuri ya Czech na Uholanzi Jumamosi ijayo ya Julai 3.

Author: Asifiwe Mbembela