Juventus yamteua Andrea Pirlo kuchukua nafasi ya kocha Sarri aliyetimuliwa

360

Muda mfupi baada ya Juventus kumtimua aliyekuwa Kocha wake Maurizio Sarri imemteua Kiungo wa zamani wa timu hiyo Andrea Pirlo baada ya kufundisha kwa muda mfupi tangu alipoteuliwa kukinoa kikosi cha wachezaji walio chini ya umri wa miaka 23.

Miamba hiyo ya soka la Italia imemtimua Sarri baada ya msimu mmoja tu akitokea Chelsea ambako alifanikiwa kuipatia taji la Europa League. Amekiongoza kikosi cha Juventus kushinda taji la Seria A ingawa amepoteza nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya kufuatia sare ya goli 2-2 dhidi ya Lyon katika mikondo yote miwili.

Pirlo, 41, amesaini kandarasi ya miaka miwili mpaka Juni 2022.

Mchezaji huyo wa zamani wa Juventus aliteuliwa kuwa kocha wa kikosi cha vijana wenye chini ya miaka 23 mwezi Julai 30 mwaka huu.

Pirlo alicheza mechi 164 ndani ya uzi wa Juve kuanzia mwaka 2011 hadi 2015 na kushinda mataji manne ya Seria A baada ya kujiunga nayo akitokea AC Milan akishinda mataji mawili makubwa ya Ulaya.

Pirlo, aliyeichezea timu ya taifa ya Italia mechi 116 na anatajwa kuwa miongoni mwa viungo bora sana duniani alistaafu mwaka 2017 baada ya miaka miwili kwenye ligi ya Marekani ndani ya New York City Fc.

Pirlo baada ya kuteuliwa amesema anatamani kuwa na maisha mazuri kwenye ukocha kama ilivyo kwa Kocha wa Manchester City Pep Guardiola na Kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane Zizzou.

Author: Bruce Amani