Mtibwa maji ya shingo, TFF yahusika

358
Baadhi ya Waandishi wa Vitabu huamini wakati mzuri wa mwanadamu kufikiria ni nyakati ambazo hukumbwa na magumu ama changamoto nyingi.
Hili unaweza kuwalinganisha na kile kinachoendelea kati ya Uongozi wa klabu ya Mtibwa Sugar na Shirikisho la Soka TFF na Bodi ya Ligi, kwani Mtibwa imekiri kuwa bado ipo njia panda kufuatia kufungiwa kwa viwanja vyake vyote ilivyokuwa inachezea mechi za nyumbani kunako Ligi Kuu Bara.
Ikiwa ni wiki kadhaa tangu kufungiwa Uwanja wa Manungu, Mtibwa ilipangiwa kutumia uwanja wa Jamhuri ambao nao wiki hii umetangazwa kufungiwa na Bodi ya Ligi kutokana na kutokidhi mahitaji ya uwanja.
Ofisa Habari wa Mtibwa, Thobias Kifaru, ameibuka na kusema kuwa hadi sasa wapo njia panda kuwa watatumia uwanja gani.
“Kiukweli hatujajua maana Manungu ilifungiwa na sasa Jamhuri nayo pia imefungiwa.
“Tunachoomba sisi TFF na Bodi ya Ligi waturuhusu tutumia huu wa Manungu sababu tunaingia kwenye gharama kubwa sana kupeleka timu Jamhuri, inakuwa kama tunaenda ugenini.
“Tunawaomba TFF watusaidie kwa hili hata kwa kipindi hiki tukiwa tunaelekea kujenga uwanja wetu wenyewe.”
Upande wa Bodi ya Ligi, kupitia Mtendaji wake Boniface Wambura alisema “Kila klabu inatakiwa kuwa na kiwanja chenye hadhi ya kuchezewa(pitch), majukwaa na huduma nyingine za kijamii kama vyoo”.
Uwanja wa Jamhuri ni miongoni mwa viwanja vingine vilivyo fungiwa awamu ya pili baada ya vile vya awali kama dimba la Mabatini Mkoani Pwani na Manungu

Author: Asifiwe Mbembela