Simba yaifumua Namungo, sasa kukutana na watani wao wa jadi Yanga fainali ya Kombe la Mapinduzi

477

Simba SC imefuzu kuingia fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya Jana usiku kuifunga klabu ya Namungo FC ya Tanzania Bara goli 2-1 katika mchezo uliopigwa dimba la Amaan Zanzibar ikiwa ni nusu fainali ya pili.

Wekundu wa Msimbazi Simba wakiwa kama mabingwa wa Kombe hilo mara tatu wanatinga hatua ya fainali na sasa watapepeta na watani wao Yanga. Simba ilianza kushinda mapema dakika ya 6 kupitia kwa Meddie Kagere baada ya kiraka, Abdulhaman Humud kujichanganya wakati wa kuokoa hatari.

Bao la pili ilikuwa ni kazi ya Miraj Athuman dakika ya 39 baada ya kutumia mpira uliopigwa na kiungo Hassan Dilunga kugonga mwamba akakutana nao ukiwa unarejea uwanjani na kuuzamisha kambani.

Namungo hawakuwa wanyonge kipindi cha pili waliwapa tabu Simba ambapo dakika ya 83 Kichuya Shiza aliingia ndani ya uwanja akichukua nafasi ya Jaffary Kibaya. Ilimchukua dakika nne kuweza kutengeneza nafasi ambapo alitoa pasi kwa kupiga faulo iliyokutana na kichwa cha Stephen Sey aliyepachika bao kwa kichwa dakika ya 87.

Simba walikuwa kwenye presha kubwa kipindi cha pili baada ya Namungo kuzinduka katka kusaka ushindi ila muda ulikamilika kwa Simba kushinda mabao 2-1. Matokeo hayo yanaifanya Simba kutinga hatua ya fainali na inakwenda kukutana na Yanga, Jumatano.

Author: Asifiwe Mbembela