Yanga yaendelea kuwasha moto hadi mkoani

100

Klabu ya Yanga imeibuka na ushindi mnono dhidi ya Tanzania Prisons “Wajela Original” kwa goli 3-1 katika mchezo uliochezwa katika dimba la Sokoine jijini Mbeya ukiwa ni muendelezo wa ligi kuu ya kandanda nchini Tanzania bara TPL.

Tanzania Prisons ambayo ilihitaji ushindi ili kujinasua katika nafasi tatu za chini lakini ilishindwa kulinda goli lililopatikana Kipindi cha kwanza kwa njia ya penalti baada ya Andrew Vincent ‘Dante’ kufanya makosa kwenye kisanduku na mwamuzi kuamru lipigwe tuta ambapo Jumanne Elfadhili  alitia kimiani mkwaju huu kunako dakika ya 45.

Yanga iliweza kuamka katika kipindi cha pili na iliwachukua dakika ya 75 kuandika goli la kwanza kupitia kwa Ibrahim Ajib ambaye alifunga kwa njia ya penati pia baada ya mlinzi wa Prisons kunawa katika kisanduku cha 18.

Aliyekuwa nyota mchezo akitokea akiba Amisi Joslini Tambwe alifunga goli lake la tatu la ligi katika dakika ya 85 baada ya kujisahau kwa mabeki wa Prisons ambao walikosa utulivu katika mchezo huo.

Haikumchukua mda mrefu mshambuliaji huyo raia wa Burundi kuandika goli la tatu kwa upande wa Yanga na goli la pili kwake ilikuwa ni 90+3 ambapo alifunga goli na kuifanya Yanga kufikisha alama 38, michezo 14 katika msimamo wa TPL.

Matokeo hayo yanaifanya Prisons kushuka zaidi nafasi moja na sasa inashika nafasi ya 20, michezo 15 juu kuna Biashara ambayo nayo Leo imepoteza dhidi ya Lipuli FC.

Katika mchezo wa leo kulikuwa na matukio mengi yaliyokuwa yakitoa picha tofauti huku wengine wakisema mechi ilimzidi uwezo mwamuzi wa mchezo huo, huku tukishuhudia kadi mbili nyekundu moja kwa Mrisho Ngassa kwa upande wa Yanga na Mpalile kwa Prisons.

 

Author: Bruce Amani