Yanga yawanyoosha wanajeshi JKT

315

Yanga iliwatandika Wanajeshi JKT Tanzania 3-0 katika mtanange wa ligi kuu ya Tanzania TPL uliochezwa dimba laTaifa mjini Dar es Salaam Alhamisi jioni.

Ushindi huo unaepeleka Yanga mpaka nafasi ya 1 ya msimamo wa TPL kwa alama 35 ikiwa sawa kimichezo na Azam yenye alama 32 zote zimecheza mitanange 13 huku Simba ikishika nafasi ya tatu kwa alama 27 ingawa ipo nyuma michezo miwili.

Magoli ya Yanga yalipatikana kupitia kwa Heriet Makambo dakika ya 20 baada ya makosa katika safu ya ulinzi, Mrisho Ngassa ‘Anko’ dakika ya 53 kupitia shuti kali lililopoteza mbawa na kumgonga Ngassa na kutimba wavuni na baadae Ibrahim Ajib Migomba akafunga goli la 3 kwa njia ya penati na kunogesha ushindi zaidi wa mabingwa hao wa kihistoria.

Baada ya mchezo huo sasa Yanga inatimiza mechi 11 bila kupoteza hata mchezo mmoja huku sare zikiwa 2 (Ndanda na Simba).

Aidha kwa upande wa JKT wanaendelea kusalia katika nafasi ya 8 wakiwa na pointi 19 ilizozipata katika michezo kumi na tatu.

Pamoja na kwamba ni mwanzo mwa msimu endapo Yanga itamaliza msimu bila kushindwa itakuwa imeingia kwenye rekodi ya Simba ya kucheza msimu mzima bila kupoteza hata mchezo mmoja. Ligi hiyo itaendelea tena wikiendi ijayo

Author: Bruce Amani