Yanga yakana tetesi kuhusu Mukoko Tonombe

479

Wiki iliyopita ilikuwa ngumu kwa Yanga hasa mashabiki baada ya kuwepo kwa tetesi kwenye mitandao ya kijamii juu ya kiungo wao mkabaji Mukoko Tonombe kuhitajika na Klabu ya Horoya ya Guinea lakini uongozi wa klabu hiyo umekana taarifa hizo.

Mukoko Tonombe aliyejiunga na Yanga akitokea AS Vita Club mwanzoni mwa msimu uliopita amegeuka kuwa nuru kikosini na uwepo wa taarifa hizo ulikuwa ni kama mwiba kwenye kidonda.

Akizungumzia juu ya tetesi hizo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema hawajui chochote kuhusu suala hilo na wenyewe wanaona kwenye mitandao ya kijamii na kwamba hawajapokea taarifa yoyote juu ya Horoya kumtaka mchezaji wao.

Bumbuli amesema kama Horoya wanamtaka Mukoko watawatafuta na kukaa nao chini kuzungumza nao lakini kwa sasa wameelekeza nguvu kwenye michezo ya Azam Sports Federation Cup na michezo ya ligi kuu.

“Hakuna hiyo taarifa kwetu kuwa Horoya wanamtaka Mukoko. Ni taarifa ambazo hata sisi tunaona kwenye mitandao ya kijamii lakini hakuna ofa yoyote, macho yetu kwa sasa tunawaza michezo yote ambayo ipo mbele yetu”.

Hata hivyo, kumekuwa na maneno kuwa mchezaji huyo aliyebakiza mwaka mmoja kwenye kandarasi yake ndani ya Timu ya Wananchi Yanga anaweza kung’oka kutokana na kitita kirefu ambacho klabu ya Horoya imetenga.

Author: Asifiwe Mbembela