Yanga yamtangaza Al Nabi kuwa kocha wao

1,550

Yanga imemtangaza rasmi kocha mpya wa kukinoa kikosi hicho Nadreddine Al Nabi baada ya aliyekuwa kocha wa klabu Cedric Kaze kufutwa kazi Machi 17 kutokana na matokeo mabaya.

Kocha huyo raia wa Tunisia mwenye asili ya Ubeligiji, anajiunga na Yanga akiwa ameambatana na makocha wasaidizi akiwemo kocha wa viungo.

Mbele ya Waandishi wa Habari katika mkutano wa utambulisho wa Mtunisia huyo ameweka wazi kwamba anaitambua Yanga kwa kuwa alikuwa anaifuatilia muda mrefu jambo ambalo halimpi tabu.

Ataungana na mzawa Juma Mwambusi ambaye kwa sasa anainoa Yanga akiwa ni Kaimu Kocha Mkuu ambapo wambusi ataongoza mchezo wa leo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Gwambina FC utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, saa 1:00 usiku.

Kocha huyo amesema: “Mimi ni kocha wa vitendo, sipendi porojo wala bla bla bla hapana kwangu ni kazi nataka Yanga iwe timu kubwa.

“Ninaijua vizuri na nina amini kwamba nitafanya vizuri hivyo ninashukuru kwa nafasi ambayo nimeipata nitatoa ushirikiano na kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema.

Yanga kwenye msimamo ipo nafasi ya kwanza ikiwa imecheza jumla ya mechi 25 na kukusanya pointi 54, leo inakutana na Gwambina FC iliyo nafasi ya 12 kwenye msimamo na pointi 30 na imecheza mechi 24.

Kocha huyo ana uzoefu na soka la Afrika kwa kuwa miongoni mwa timu ambazo alifundisha ni pamoja na Al Merrikh ya Sudan ambayo iliishia hatua ya makundi, Ligi ya Mabingwa Afrika.

Author: Asifiwe Mbembela