Nyota wa Simba Manula, Bocco kuikosa FC Platinum Ligi ya Mabingwa

274

Kocha Mkuu wa kikosi cha Simba Sven Vandenbroeck amesema nyota wake wawili wataikosa mechi ya kesho Jumatano dhidi ya FC Platinum kutokana na majeruhi ambayo wameyapata wakiwa katika maandalizi ya mchezo huo.

Sven ambaye alichukua mikoba ya Patrick Aussems amewataja nyota hao kuwa ni John Bocco nahodha wa timu na kipa namba moja Aishi Manula na kusema wote watakosa mtanange huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya pili.

Sven amesema: “Tuna masaa machache kabla ya mchezo, tumejaribu kila kitu ili wawe tayari kwa mchezo lakini itakuwa ngumu kuwa tayari.

“John [Bocco] bado yupo kitandani hayupo sawa, Aishi aliumia mchezo uliopita na anaweza kuchukua wiki au zaidi ili kuwa sawa. Mpaka sasa kuna uwezekano asilimia 50 ya kuwepo kwenye mchezo.”

Ikiwa Manula hatakuwa fiti mpaka kesho mikoba yake inaweza kuchukuliwa na Ally Salim ama Beno Kakolanya.

Hata hivyo, bado kuna walakini juu ya kauli za kocha huyo kwa wachezaji hao kuukosa mchezo kwani mara kadhaa tathimini yake kabla ya mchezo imekuwa tofauti na uhalisia.

Author: Asifiwe Mbembela