Bayern yaiongezea Dortmund joto kileleni mwa ligi

150

Borussia Dortmund, kazi kwenu! Bayern Munich imewaongezea joto Borussia Dortmund baada ya kupata ushindi wa 1 – 0 na kuwafikia vinara hao wa Bundesliga. Bayern sasa wana pointi 51 sawa na Dortmund ambao wana mchezo mkali Jumapili dhidi ya Bayer Leverkusen.

Kiungo Javi Martinez, ambaye alicheza safi sana katika sare ya 0 – 0 dhidi ya Liverpool kwenye Champions League alikamilisha wiki nzuri kwake kwa kufunga bao hilo pekee na la ushindi katikati ya kipindi cha pili.

Bayern ambao wakati mmoja walikuwa nyuma ya BVB na pengo la pointi tisa, wamekamata nafasi ya pili pointi sawa na Dortmund lakini na tofauti ya mabao. Dortmund wanaweza kurejesha pengo la pointi tatu kama watawabwaga Leverkusen lakini nahodha Marco Reus yuko nje kutokana na jeraha. BVB wameshindwa kupata ushindi wa mechi tatu za ligi wakati Leverkusen wameshinda mechi nne mfululizo.

Matatizo ya Schalke yazidi

Schalke, ambayo ilipoteza 3 – 2 dhidi ya Manchester City kwenye Champions League, ilipata kipingo kingine cha 3 – 0 dhidi ya Mainz, timu ambayo ilikuwa imepoteza mechi zake tatu za ligi.

Schalke pia ilitangaza kuwa mkurugenzi wa kimichezo Christian Heidel ataondoka mwishoni mwa msimu huu. Heidel alipata mafanikio katika wadhifa huo akiwa Mainz, lakini amekumbwa na shinikizo kali kutokana na matatizo ya Schalke msimu huu. Timu hiyo ya kocha Domenico Tedesco ipo katika nafasi ya 14 kwenye ligi yenye timu 18.

Ngome yavunjwa

Nambari tatu kwenye ligi Borussia Moenchengladbach walikuwa wameshinda mechi zao zote za nyumbani msimu huu, hadi Hertha Berlin walipata ushindi wa 3 – 0 mnamo Februari 9. Wolfsburg walihakikisha  Galdbach wanapata kipigo cha pili mfululizo cha 3 – 0 nyumbani shukrani kwa mabao mawili kutoka kwa Admir Mehmedi.

Author: Bruce Amani