Gor Mahia yawalaza Lobi Stars katika mchuano wa CAF

148

Mabingwa wa ligi ya kandanda nchini Kenya Gor Mahia wamefanikiwa kuanza vyema kampeni za kuwania ubingwa wa klabu bingwa Afrika baada ya kuishindilia klabu ya Lobi Stars kutokea Nigeria 3-1 katika mchezo wa raundi ya kwanza uliofanyika uwanja wa kimataifa wa Moi Sports Center (MISC), Jumapili hii Disemba 16. 

Wenyeji walionekana kuutawala mchezo tangu dakika za awali hasa baada ya mshambuliaji Jacques Tyusenge kufunga goli dakika saba za mchezo kupitia mgongea kutoka kiungo Francis Kahata. 

Samuel Onyango aliifungia goli la pili Gor Mahia katika dakika ya 21 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Tyusenge aliyeonekana kuwa mchezaji hatari kwenye mtanange huo, ingawa baadae Lobi walipata goli la kufutia machozi kupitia kwa Samad Kadiri.

Mlinzi wa zamani wa timu ya Ulinzi Stars Onyango alifunga goli la tatu kwa Gor Mahia na goli la pili kwake na kufanya mchezo huo kuwa 3-1.

Tyusenge ambaye ni raia wa Rwanda na mwezake Onyango (Kenya) walikosa nafasi nyingi za wazi ambazo zingezaa magoli mengi zaidi. Timu hizo mbili zitarejea dimbani wiki moja kutoka sasa.

Author: Bruce Amani